BREAKING NEWS

VIDEO

BIASHARA

USHAURI WETU

Saturday, March 5, 2016

WANAWAKE NA FURSA-UJUMBE KWA WANAWAKE WA TANZANIA 8 MACHI, 2016

Tanzania ni mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki – Kutokana na milango kuwa wazi sasa Mheshimiwa Rais wetu Magufuli ametuhakikishia tunaweza kuvuka mipaka na kujitanua kupata fursa zaidi. Katika kuadhiminisha siku ya wanawake Duniani - Wanawake wa Tanzania tuinuke na tujihakikishie kushiriki kikamilifu katika ubunifu wa biashara endelevu ambazo zitakuwa na viwango vya kukidhi matakwa ya kijumuiya, tuache kutengeneza bidhaa za kuishi muda mfupi na zisizo na ubora. Fursa zinatutembelea tuwe wasomaji wa magazeti na vitabu hata mitandao ya kijamii ili tuweze kujipatia mbinu za kutengeneza na kuuza  bidhaa za aina mbalimbali ambazo ni za kwetu wenyewe na sio kuchat na kudadisi tu kupitia mitandao muda wote, tuitumie hii mitandao kwa manufaa ya kutangaza biashara zetu wenyewe. “HAPA KAZI TU”.

Tumehakikishiwa kwamba bidhaa za ndani sasa zimepewa kipaumbele, ebu tuamke na kukimbilia Taasisi za fedha kama vile CRDB, NMB, NBC, EXIM, BOA, POSTA, FINCA, BLACK na BLUE na Taasisi zingine za fedha kuweza kuchukua mikopo yenye tija kwa uzalishaji wa uhakika.  Wanawake tunaweza sana, tuache hofu na uoga wa kushindwa.  “Sikuzote  asiyekubali kushindwa sio mshindani”.

Maisha ili yawe mepesi wanawake  tunatakiwa tujitoe kwa hali na mali, kinamama tuwe mfano kwa kizazi kijacho kwa kujihakikishia tumejipanga kufika mbali katika biashara zetu ili kuinua uchumi wetu na familia zetu. Tukifanya biashara zetu sisi ndio tutakaoweza kuwaandalia watoto wetu maisha mema na yenye tija. Tunaweza kuchangia madawati, madaftari na vitabu vya kiada vya watoto na huduma nyingine nyingi katika jamii yetu. Kwani ukimwelimisha mwanamke umeielimisha jamii nzima na pia kila mwanaume aliyefanikiwa nyuma yake kuna mwanamke.  Tunalilia usawa basi na tukimbilie fursa kwa usawa.

Tanzania wanawake ni wengi sana hasa wafanyakazi na wafanyabiashara, kwa wale waliofanikiwa tuwafundishe wengine mbinu za kuweza kujiinua kwa urahisi na kufikia malengo. Maarifa ukimgawia mwingine unafanikiwa zaidi tuondoe ile hari ya wivu na masengenyo wakati wote sisi kwa sisi.  Tuwe tayari kuwauliza wanawake waliofanikiwa njia gani wamepita au wanapitia ili tuweze kujifunza kupitia wao.  Wanawake tuwe wazuri katika kurejesha mikopo katika Taasisi za fedha kwani wanawake wengi wanakopa na kukimbilia Taasisi nyingine na kuacha madeni yasiyolipika. Mafanikio hayakimbiwi ila mafanikio yanakimbiliwa.

Naamini ujumbe huu utawafikia wanawake wa Tanzania nzima ili tuamke na kuchangamkia fursa zozote zinazojitokeza kwa kipindi hiki cha “HAPA KAZI TU” kwani asiyefanya kazi na asile.

Wanawake tunaweza.

Lusako Mwakiluma
MKURUGENZI WEZESHA TRUST FUND


Post a Comment

 
Copyright © 2013 WEZESHA TRUST FUND
Powered by WordPress24x7