Tanzania ni mwanachama
mwaminifu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki – Kutokana na milango kuwa wazi sasa Mheshimiwa Rais wetu Magufuli ametuhakikishia tunaweza kuvuka mipaka na kujitanua kupata fursa zaidi.
Katika kuadhiminisha siku ya wanawake Duniani - Wanawake wa Tanzania tuinuke na
tujihakikishie kushiriki kikamilifu katika ubunifu wa biashara endelevu ambazo
zitakuwa na viwango vya kukidhi matakwa ya kijumuiya, tuache kutengeneza bidhaa
za kuishi muda mfupi na zisizo na ubora. Fursa zinatutembelea tuwe wasomaji wa
magazeti na vitabu hata mitandao ya kijamii ili tuweze kujipatia mbinu za kutengeneza
na kuuza bidhaa za aina mbalimbali
ambazo ni za kwetu wenyewe na sio kuchat na kudadisi tu kupitia mitandao muda
wote, tuitumie hii mitandao kwa manufaa ya kutangaza biashara zetu wenyewe. “HAPA KAZI TU”.
Tumehakikishiwa kwamba bidhaa
za ndani sasa zimepewa kipaumbele, ebu tuamke na kukimbilia Taasisi za fedha
kama vile CRDB, NMB, NBC, EXIM, BOA,
POSTA, FINCA, BLACK na BLUE na Taasisi zingine za fedha kuweza kuchukua
mikopo yenye tija kwa uzalishaji wa uhakika.
Wanawake tunaweza sana, tuache hofu na uoga wa kushindwa. “Sikuzote
asiyekubali kushindwa sio mshindani”.
Maisha ili yawe mepesi
wanawake tunatakiwa tujitoe kwa hali na
mali, kinamama tuwe mfano kwa kizazi kijacho kwa kujihakikishia tumejipanga kufika
mbali katika biashara zetu ili kuinua uchumi wetu na familia zetu. Tukifanya
biashara zetu sisi ndio tutakaoweza kuwaandalia watoto wetu maisha mema na
yenye tija. Tunaweza kuchangia madawati, madaftari na vitabu vya kiada vya
watoto na huduma nyingine nyingi katika jamii yetu. Kwani ukimwelimisha
mwanamke umeielimisha jamii nzima na pia kila mwanaume aliyefanikiwa nyuma yake
kuna mwanamke. Tunalilia usawa basi na
tukimbilie fursa kwa usawa.
Tanzania wanawake ni wengi
sana hasa wafanyakazi na wafanyabiashara, kwa wale waliofanikiwa tuwafundishe
wengine mbinu za kuweza kujiinua kwa urahisi na kufikia malengo. Maarifa
ukimgawia mwingine unafanikiwa zaidi tuondoe ile hari ya wivu na
masengenyo wakati wote sisi kwa sisi.
Tuwe tayari kuwauliza wanawake waliofanikiwa njia gani wamepita au
wanapitia ili tuweze kujifunza kupitia wao.
Wanawake tuwe wazuri katika kurejesha mikopo katika Taasisi za fedha
kwani wanawake wengi wanakopa na kukimbilia Taasisi nyingine na kuacha madeni yasiyolipika. Mafanikio hayakimbiwi ila mafanikio
yanakimbiliwa.
Naamini ujumbe huu utawafikia
wanawake wa Tanzania nzima ili tuamke na kuchangamkia fursa zozote
zinazojitokeza kwa kipindi hiki cha “HAPA
KAZI TU” kwani asiyefanya kazi na asile.
Wanawake tunaweza.
Lusako Mwakiluma
MKURUGENZI WEZESHA TRUST FUND
Post a Comment