BREAKING NEWS

VIDEO

BIASHARA

USHAURI WETU

Friday, January 20, 2017

WEZESHA TRUST FUND WALIPOFANYA ZIARA KWA WAHANGA WA MAFURIKO WILAYA YA KILOSA MEI, 2016

Wafanyakazi wa Wezesha Trust Morogoro walipotembelea Wilayani Kilosa kuwapa pole wahanga wa mafuriko Wilayani Kilosa.  Mafuriko hayo yalitokea mwanzoni mwa mwaka 2016.  Wezesha ilitoa pole kwa misaada ya nguo, chakula na pesa taslimu.  Pia Wezesha walienda kuangalia eneo lililoathirika na mafuriko kijijin na mto wa Tindiga ambao ni  chanzo cha mafuriko.
                               
Mkurugenzi wa Wezesha Trust Fund Bi Lusako Mwakiluma akikabidhi misaada kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mheshimiwa Henjewele Mei, 2016, misaada iliyokabidhiwa ni chakula, nguo, fedha taslimu na vitu mbalimbali.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya Henjewele akishukuru Asasi ya Wezesha na wadau wote waliochangia hali na mali kuhakikisha misaada inapatikana na kupelekwa Kilosa kwa wahathirika wa mafuriko.  Mungu awabariki wote waliotoa kwa upendo misaada hiyo.

Wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa wakishusha misaada toka kwenye gari baada ya Wezesha kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kilosa.  Aliyekuwa Katibu Tawala wa Wilaya aliongoza ushushaji wa misaada hiyo.
Wafanyakazi wa Wezesha Trust Fund walipokuwa Kilosa mara baada ya kukabidhi misaada hiyo kwa Mkuu wa Wilaya kutoka kushoto Mohamed Nyongo(Kaimu Afisa Mafunzo), Janeth Lupupa(Afisa Mafunzo) na Abuubakari Mkingiye(Mratibu wa mambo ya nje) wanaiomba jamii kujitoa kwa hali na mali katika matukio yoyote yanayowahusu watu wengine kwani wanaamini kutoa ni moyo wala sio utajiri.

Wafanyakazi wa Wezesha wakitathmini athari za mafuriko katika nyumba za wenyeji ambao walizikimbia baada ya mafuriko kutokea kutoka kulia ni Mohamed Nyongo(Kaimu Afisa Mafunzo) na Salum Tindwa(Mratibu wa Miradi) Wezesha Trust Fund.  Kwa kweli hali ilikuwa ni mbaya lakini Mungu amesaidia wahathirika wako sehemu sahihi kwa muda huu.

Nyumba iliyoathirika na mafuriko ikiwa imeezuliwa paa na uharibifu mkubwa, maji yaliingia ndani ya nyumba kiasi cha 3/4.

 Watoto walioathirika na mafuriko wakiwa wanacheza eneo la tukio kwani imekuwa kama jangwa, mazao yalipotea, mkondo wa maji umeharibu shule, makanisa na hata sehemu za watoto kucheza.
 Wamama waliothirika na mafuriko wakiwa wanatoka kuchota maji mbali na makazi yao, kisima cha maji kilizibwa na matope makali  na ikafikia mahali maji yalikuwa shida, lakini Mungu ni mwema wameviona baadhi ya visima na wanaendelea na maisha mahali hapo.

Wezesha Trust Fund inawaomba watanzania, wanajamii  na wadau wote kwa ujumla kujitoa kwa uadilifu katika kila janga linalowapata wenzetu.  Jamii yetu ni wamoja tupendane na kutendeana yaliyo mema na Mungu wa Mbinguni atatulipa.

Lusako Mwakiluma
Mkurugenzi 



Wednesday, January 18, 2017

JE, UTAWEZAJE KUSHINDA HALI NGUMU YA MAISHA NA AJIRA




MBINU 6 ZITAKUSAIDIA SANA
Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na hali ya kukua kwa uchumi mambo mengi yamebadilika sana, Hivyo basi ni muhimu tujifunze njia za kujiimarisha ili tuweze kupita salama katika hali hii, usipoteze muda kulalamika amka anza kuangalia mbinu hizi ili uboreshe maisha yako.  Nenda na dira usiwe mchelewaji wah sana uone faida ya kuwa wa kwanza katika kutatua matatizo na kupata fursa zilizopo karibu uone mbinu ambazo zitakusaidia kuinuka kiuchumi kwa haraka.

1. Uhuru wa fikra:  Kama kuna nyakati ambapo unahitaji uwezo wa kuiona dunia kama ilivyo na sio kama unavyotaka iwe, basi ni sasa. Ni muhimu kuboresha ufahamu wako wa mambo mengi ya kimsingi ya kimaisha kama vile mapenzi, biashara, tabia, teknolojia ,, na zaidi sana  maswala ya kiroho.
Uhuru wa kifikra utakuwezesha uweze kujitawala vema, kwani kimsingi wewe ndiye mtu wa kwanza kabisa unayeweza kuleta mabadiliko makubwa na maendeleo kwa maisha yako, kwakuwa unayo nguvu ya utashi,  kufanya maamuzi au kuacha watu waamue mambo kwa ajili yako.

2. Kuboresha mtandao:  Kwakuwa unahitaji kutambua fursa nyingi kwa kadri inavyowezekana na kwa kuwa wewe ni mzalishaji, unahitaji sana kujenga mtandao mkubwa na mtandao wenye manufaa ili kuweza kutambua fursa mbalimbali kupitia mtandao wako, na pia kuweza kuuza bidhaa zako kupitia mtandao huo.  

3. Kuwa mzalishaji: Katika machafuko haya, bidhaa na huduma mbalimbali zitakuwa adimu, na kwa wazalishaji wachache watakaoweza kuzalisha kwa ufanisi wataweza kujikuta wakiendesha maisha vizuri.  Hivyo pamoja na kuwa mtumiaji wa fedha zako kwa mambo ya burudani, unahitaji kuhifadhi fedha zako kwa namna ambayo fedha zako hazitopoteza thamani zake, na wakati huo huo, ukifanya utafiti wa aina ya bidhaa au huduma ambazo utakuwa ukizalisha, ili nawe unufaike na mazingira tuliyonayo.  Kuendelea kuwa muingizaji wa kipato (kwa njia ya ajira pekee) na kuwa mtumiaji zaidi ya mwekaji akiba, si jambo la busara, hasa katika hali ngumu ya kiuchumi na kijamii tuliyonayo.

4. Kuwa mwepesi wa kubadilika: Mambo mengi yanabadilika kwa haraka sana, ufahamu uliokuwa nao jana , mbinu ulizotumia siku za nyuma  hata kama zilifanikiwa, inawezekana kabisa zisifanikiwe kwa sasa, na kwa kadri mambo yanavyozidi kubadilika. Ushindi wa kipekee unakuja pale unapoweza kuwa mwepesi wa kubadilika, kwa kubuni njia mpya na bora za kukabiliana na mazingira unayokumbana nayo.

 

5. Kaa tayari kwa kusafiri:  Fursa zinaweza kutokea popote pale, hivyo kuwa tayari kusafiri nje ya mkoa uliopo sasa, na zaidi sana nje ya nchi. Hakikisha una passport halali na isiyoisha muda wake, na tambua taratibu za kusafiri nje ya nchi, kama vile mambo ya visa,  na gharama za maisha kwa nchi tofauti.  

6. Mipango ya muda mrefu: Tambua kuwa hali hii ngumu ya maisha ni swala ambalo litaendelea kwa muda mrefu, hivyo ni muhimu kujipanga wewe na familia yako. Kama una watoto au una mpango wa kuwa na watoto, basi ni wakati wa kufikiria pia namna ya kuja kuwawezesha watoto wako wawe na ujuzi wa uhakika, na kuwa wawe wazalishaji.  Hakikisha unajitengenezea ujuzi na uzoefu uliokomaa katika jambo fulani au mambo kadhaa tofauti, ili uweze kuja kuuza ujuzi na uzoefu wako huo katika soko gumu la huduma tunalokumbana nalo kwa nyakati za leo na zijazo.

Lusako Mwakiluma
Muhamasishaji na Muinuaji
January, 2017


Sunday, January 1, 2017

SABABU ZINAZOPELEKEA WANAWAKE KUWATEGEMEA WANAUME JAPOKUWA WANA FURSA NYINGI SANA

Fursa za wanawake  ziko nyingi sana lakini wanawake wenyewe hawana motisha ya kuzikimbilia na kwenye uzalishaji mali wako vizuri sana ila tu kuna baadhi ya wanawake ni waoga kujaribu nab ado wanaamini kuwa mwanaume ni mtafutaji na mwanamke ni mama wa nyumbani siku zote.  Hii inaonyesha mwanamke akiishi bila mume  au akikimbiwa na mwanaume anashindwa kusimama kwa hofu  ya kushindwa maisha.  Kuna fursa za kibiashara, ufugaji na utengenezaji bidhaa mbalimbali ambazo kila siku zinajitokeza lakini katika suala la kujifunza wanawake ni wazito na hata kuuliza kama kitu hawawezi pia ni taabu.

Wezesha Trust Fund inatumia njia nyingi katika kuwaelimisha wanawake:  Inatumia Television, Redio, semina na warsha za mara kwa mara. Wanawake wengi  wanatambua kuwa kila mwanaume aliyefanikiwa nyuma yake yuko mwanamke na ukikuta mwanamke kafanikiwa ujue nyuma yake yuko peke yake.  Wanawake pia wana majukumu mengi ya kifamilia na ya kibiashara, apike, afue, aende kazini, anyonyeshe na pia amhudumie mume na watoto.  Muda wake ni ule ule na kazi ni nyingi, kuna muda anachoka kwani naye ni binadamu.

Wakati naongea na wanawake hawa nakutana na changamoto nyingi wanazopitia wanalalamika wenyewe kwamba hawajiamini, waoga, na wakiona biashara kidogo zinasumbua wanaacha.  Na kuna wengine mitaji inakata kwa sababu ya waume zao wanawaachia majukumu ya nyumbani na pia wanaume hao hao hawawapi fursa wanawake zao za kufanya biashara kwa upana zaidi. Pia wengine wanawakataza wasitoke majumbani kwenda kwenye biashara.  Wapo wanawake wengine wao makundi yanawaharibu wanaishi maisha ya kuiga na kutamani vitu nje ya uwezo wao.

Ushauri wangu adui wa mwanamke ni yeye mwenyewe na pia kutokana na mfumo  uliopo tangu awali  wanawake ni viumbe hafifu na wengi wanafahamu hivyo na hawataki kuchukua hatua, wainuke na waseme hapana inapobidi kusema hapana. Wanaume nao nawaomba waache kuwakatisha tamaa wake zao  bali wawatie moyo kwani wanawake wakitiwa moyo na nguvu wana ujasiri kuliko hata wanaume, pia kuna wakati wawasaidie majukumu ya nyumbani kama yanakuwa mengi.  Pia wanawake ni wazuri katika kutunza fedha.  Nawaomba wanawake wenzangu wajidhatiti katika kusimamia kile walichonacho ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea ya maendeleo.  

Wezesha na wadau wengine hatutaacha kuwatia moyo wakati wote watakapohitaji ushauri wa kitaalamu. Kauli Mbiu yetu siku zote: “Wakiwezeshwa wanaweza

Karibuni tulishirikiane kulijenga Taifa letu kwa bidii na maarifa.

Lusako Mwakiluma

Mhamasishaji na muinuaji waliokata tamaa
 
Copyright © 2013 WEZESHA TRUST FUND
Powered by WordPress24x7