BREAKING NEWS

VIDEO

BIASHARA

USHAURI WETU

Monday, February 29, 2016

MAISHA NI RAHISI SANA UKITULIA NA KUTAFAKARI

Napenda kutoa mada fupi na ya kutiana moyo wenyewe kwa wenyewe, kwa mtazamo wa macho ya nyama maisha ni magumu sana, lakini katika mtazamo wa kiroho maisha ni ya kawaida na hayataki mashindano, unashindana na nani? Na unaishi kwa ajili ya nani?  Fanya kile kitu kina manufaa kwako na familia yako ili kesho uje uburudike.  Kwani kuishi ni leo kesho ni matokeo unaweza ufike au usifike, jiwekee akiba kama vile vile unaishi milele halafu muofie Mungu kama vile unaondoka(kufa) leo.

Watu wengi wamechukua muda mrefu kutafuta furaha wameikosa, furaha inaanzia ndani mwako (happiness is inside job) usikae ukisubiri mtu kukupa furaha, utapata ya muda, jiangalie unataka nini na unaweza kufanya nini katika maisha yako?  Jitume sana, fanya sana kazi ili uweze kula matunda mema ya nchi.  Na kumbuka tunaufukuza upepo inabidi tuweze kumshukuru huyu anayetupa pumzi ya bure kwa neema na rehema zake, wengi wanalia, wengi wamekata tamaa, wengi wanataka kujiua na wengine wamesusa hata kuanza tena kwa kuanguka.  Mwenye haki wa Mungu huwa anaanguka mara saba kisha anainuka tena.  
"With God there is second chance"

La hasha wakati ni huu tuamke na tutende yale tuliyoyandika kwenye vitabu vyetu kama ni malengo ya mwaka 2016 najua kuna wengine hawajaandika.  Maandishi yanadumu milele, mazungumzo ni muda mfupi tumia muda wako kuandika malengo yako na uyafanyie kazi.
 "see it, believe on it then you should act on it and you shall see the results as soon as possible"

Hii ni changamoto kwani kila siku angalia umefanya nini na ikifika jioni piga mahesabu ya masaa uliyotumia  kwa kufanya kitu hata kimoja cha maana.

Wako muuinuaji na mtia watu moyo hata kwa yale yanayoonekana magumu, imani pasipo kuona.

Lusako Mwakiluma


Tuesday, February 9, 2016

CHANGAMOTO KWENYE UJASIRIAMALI NA SULUHISHO

Ndugu rafiki, miezi kumi nilipo anza hii biashara nilikumbana na vitu vizito sana katika kuyafikia mafanikio na malengo niliyo lenga ningeyafikia haraka ndani ya biashara ya mtandao!
Nilijaribu kutumia mbinu mbali mbali ambazo kila mfanya biashara wa kawaida hufundisha ktk masomo ya kila siku;
��Niliambiwa ANDIKA MAJINA 100 KISHA TUMA KWA WATU WAKO WOTE UTAPATA MAJIBU MAZURI.
Nilijaribu lakini kilichonipata kiliniidhoofisha zaidi.
��Niliambiwa kila siku nishirikishe watu 5 kwa mwezi nitakuwa na watu 150. Nilijaribu lakini sikupata matokeo mazuri
��Niliambiwa kila siku nitume post moja facebook, nilituma sikuwa napata like hata moja na sikuweza kutengeneza matunda yoyote tofauti na kupoteza muda!


HIZO NI BAADHI YA MBINU NILIZO FUNDISHWA LAKINI SIKUWEZA KUPIGA HATUA KABISA KIBIASHARA. 


Ni dhahiri kuwa wengi tumekuwa tukijiunga na biashara ya mtandao na kuanza,kukimbilia RAFIKI,NDUGU ,JAMAA MBALI MBALI AMBAO TUNA MAZOEA NAO.
��Hilo sio SOKO lililokusudiwa kukupa uhuru wa kipato, ni soko ambalo SIO LA KUDUMU MAISHANI MWAKO!
KATIKA MADA ZETU TUTAKAZO JIFUNZA NI PAMOJA NA KUJUA NAMNA YA KUTENGENEZA KIPATO KISICHO KUWA NA KIKOMO KUTOKA KWENYE SOKO LILILOSAULIKA.
Kuna njia kuu mbili za kutengeneza pesa ndani ya biashara ya mtandao baada tu ya kujiunga
1. Watu ambao tayari wameshajiunga na biashara hii ya mtandao, ndani ya kampuni yako au kampuni nyingine.
Kuna njia ambazo ni rahisi ambazo zitakusaidia kupunguza gharama na kukupa faida kubwa ambayo usingetegemea kuipata!
2. Watu ambao WANATAFUTA FURSA YA BIASHARA YA MTANDAO.
Ni watu wengi wanatafuta fursa hii kila kukicha, hivyo ni jukumu lako mkufunzi kumwonesha mteja wako kuwa unaweza kumfikisha katika ndoto.
Unajua mteja HUCHAGUA MTU GANI?
~Huchagua kiongozi ambaye atamfikisha kwenye ndoto zake na kuishi maisha ya ndoto zake
~Huchagua mtu mwenye UTAJIRI WA MIFUMO HALALI YA KIBIASHARA AMBAZO ZINAKATA GHARAMA NA KUONGEZA FAIDA!
Sio hivyo tu unaweza kupanua kipato chako rafiki, KUMBUKA UNAPOJIUNGA UTAKUTANA NA ASILIMIA 98 YA SOKO LAKO (MARAFIKI ULIOTARAJIA KUWASHIRIKISHA) TAYARI WANA BIASHARA ZAO.
Tuta kufundisha namna ya kutengeneza kipato chako kwa kutatua changamoto za WAFANYA BIASHARA WENGI KUWA NA KIPATO KINACHOPITILIZA CHOTE KWENYE MATUMIZI NA KUTOKUWA ENDELEVU.
Nina imani utafurahia ukitatua hili na hebu fikilia ni WANGAPI WANALALAMIKA NA HILI KATIKA JAMII YAKO?
WENGI SANA, NDIVYI HIVYO HIVYO UTAKAVYOTENGENEZA KIPATO KIKUBWA KWA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WATU ZINAZO WAKUMBA KUHUSU ELIMU YA PESA!
Nitafurahi kuungana nami kuweza kutumiza ndoto zako kwa kuungana nami

Monday, February 8, 2016

MAMBO SITA YANAYOWEZA PELEKEA UMASKINI

 
Watu wengi wanakufa masikini na wanashindwa kufikia mafanikio yao bila wao kujua tatizo ni nini,imekuwa kama ugonjwa watu wengi kuendelea kulalamikia serikali au wazazi wao kuwa wao hawafanikiwi wao ndio sababu,na wengine wamekuwa wakikata tamaa kabisa ya mafanikio yao bila wao kujua nini kinachokwamisha maisha yao kuwa bora.Leo tutajifunza pamoja vizuwizi vya mafanikio yako ambapo kama utavifanyia kazi basi utaanza kushuhudia mafanikio yako,ni muujiza mkubwa sana utatokea kwako hakuna aliezaliwa kuwa masikini rafiki.soma kwa makini.

1.UOGA(Fear)
Hichi ni kikwazo kikubwa sana kwa watu wengi ktk mafanikio yao,watu wengi wamekuwa masikin na wengine kufa masikin kwasababu ya uoga,uoga wa kukataliwa na uoga wa kushindwa,kama unataka kufanikiwa ktk kila kitu kwenye maisha yako usiogope kuomba au kusema chochote mbele ya watu eti kwa kuogopa kukataliwa rafiki usiusemee moyo wa mwenzio usiogope,lkn pia usiogope kushindwa yani mtu anataka kufanyabiashara lkn kitu  cha kwanza anawaza ni kushindwa anaamini kuwa yeye hawezi na akianzisha atafeli.Rafiki acha uoga kwani huo ndio umasikin wako ushinde uoga ushinde maishani.USIOGOPE..
2. KUKOSA MSUKUMO (Lack of agressivenes)
Watu wengi wanashindwa kufanikiwa ktk maisha yao kwa sababu ya kukosa msukumo binafsi,ngoja nikwambie rafiki hakuna mtu yeyote ambae atakaa chini na kupanga maisha yako au kuna mtu ataacha shughuli zake kwaajili ya kupigania maisha yako,wewe ndio unaejua ugumu na uchungu wa maisha yako amka sasa kuwa na msukumo kutoka moyoni mwako wa kushinda maishani usisubiri fulani ndo akwambie nenda kazi,fanyabiashara wewe mwenyewe kaa chini jitume utafanikiwa.
3.UJASIRI NA KUJIAMIN (Courage and confidance) 
Hpa ndipo balaa watanzania wengi hawajiamini rafiki hebu jiamini kuwa wewe unaweza ndani yako kuna mtu mkubwa saana,hebu acha kusikiliza watu wengine wanasema nini kuhusu wewe usikilize moyo wako      unasema nini kuhusu wewe,usikubali kushindwa thubutu kwa kila jambo unaloambiwa lenye mafanikio na usiamini kuwa wewe huwezi unaweza rafiki.
4.KUKOSA LENGO MAALUMU (Lack of purpose driven goals)
Rafiki malengo yako nini? Lengo ni ndoto zenye mipaka,kuna malengo ya muda mfupi,muda mrefu na muda wa kati.wewe malengo yako ni yapi? rafiki hautakuja kufanikiwa ktk maisha yako kama huna malengo ya maisha yako kama huna malengo panga leo yaandike malengo yako.mtu asiye na malengo ni sawa na mtu ambae anaenda stendi kupanda gari lkn hajui anaenda wapi sasa atapanda gari gani na atashukia wapi huyu hata fika bali atazunguuka a ari hadi usiku gari linapokwenda kupaki basi litamshusha popote.JUA MALENGO YAKO RAFIKI UTAFANIKIWA.
5.KUTOKUJITOA (Lak of comittment)
Kujitoa limekuwa tatizo kwa watanzania wengi, ewe mtanzania jitoe kwaajili ya maisha yako acha uvivu wa kufikiria Mungu ashughuliki na wavivu jitoe pambana kwaajili ya maisha yako utafanikiwa. 
6.KULINDA MUDA (Timemanagement)
Hahahahaaaa watu wengi wanaposikia mua ni mali huwa hawaamini leo nataka ujue kuwa muda wako ndio umasikini wako na ndio utajiri wako.unatumiaje muda wako ambao unatoka kazini? unatumiaje muda wako ambao unatocha chuo? wewe mama wa nyumbani unatumiaje muda wako ambao unakuwa hauna kazi nyumbani? hapa ndipo kasheshe na umasikini wa watu ulipo.iko kila sekunde na saa inayopita lazima uhakikishe unafanya kitu ambacho chenye manufaa kwenye maisha yako,mfano ukitumia masaa mawili unajifunza kitu chenye mafanikio kwenye maisha yako basi unayavuta mafanikio yako masaa mawili kama mafanikio yako yalikuwa uyafikie kwa siku mbili na masaa mawili basi utakuwa umebakisha siku mbili.kama unatumia muda wako kuangalia TV,kupiga umbea kupiga story zisizokuwa na maana ukifanya hivyo masaa mawili kwa siku ndani ya mwaka utakuwa umepoteza zaidi ya miezi 4,basi hiyo miezi minne ndio umesogeza mbele mafanikio yako.kwaiyo kama ungetakiwa ufanikiwe kwa miaka miwili basi utafanikiwa kwa miaka miwili na miezi minne.sasa watanzania wengi huwa wanapoteza zaidi ya miezi 9 kila mwaka ndani ya miaka 15 tayari ameshasogeza mbele mafanikio yao kwa zaidi ya miaka kumi.kwa hiyo ukichukuwa miaka kumi ya kutafuta maisha na ile miaka kumi aliopoteza ni miaka 20.ameanzakutafuta maisha na miaka 30-40 miaka ya kufikia mafanikio yake itakua 50 na maisha now ni mafupi hayafiki huko na kipindi anaendelea kutafuta anapoteza tena masaa kadhaa.lazima ufe masikini.amka sasa mtanzania acha kutumia muda wako vibaya kwani muda wako unaoupoteza sasa utakugharimu.
MUDA NI MALI UKIPUUZA HILO UTAKUFA MASIKINI.ACHA KULALAMIKA CHUKUA HATUA.
Karibu tutimize ndoto zetu pamoja.
SOURCE:BASSANGA CHANGING LIFE

Wednesday, February 3, 2016

WEZESHA & VIYOSO IKIWAWEZESHA VIJANA WAISHIO KATIKA MAZINGIRA MAGUMU - MKOANI MOROGORO

Vijana waishio katika mazingira magumu wakijifunza kutengeneza batiki kwa kutumia mishumaa kwenye semina ya ujasiriamali tarehe 28-29/11/2013 - Sabasaba Mkoani Morogoro - waandaaji wa kuwawezesha walikuwa Wezesha Trust Fund & Victory Youth Support Organization.


Mwalimu Mama Mayala kutoka Dar es Salaam akifundisha jinsi ya kutengeneza batiki huku vijana wakiwa makini kumsikiliza, vijana hao (30) walifundishwa jinsi ya kufuga kuku wa nyama na mayai, kutengeneza chakula cha kuku, mishumaa ya aina zote na jinsi ya kuandaa vitalu na kilimo cha matunda na mbogamboga

Tuesday, February 2, 2016

MKURUGENZI WA WEZESHA TRUST FUND AKIWAFUNDISHA VIJANA WAISHIO MAZINGIRA MAGUMU JINSI YA KUTAMBUA FURSA(KIJANA JITAMBUE KUNA FURSA MBELE YAKO)


Wezesha Trust Fund & Victory Youth Support Organization kwa pamoja wamefanya kongamano la vijana waishio katika mazingira magumu Mkoani Morogoro lenye dhima "KIJANA JITAMBUE KUNA FURSA MBELE YAKO" kongamano lilifanyika katika Ukumbi wa UNGO(Umoja wa Asasi sizizo za kiserikali) Jengo la CCM Mkoa wa Morogoro.  Vijana arobaini na 48 walihudhuria na wamejifunza mambo mengi yenye maana katika maisha yao kati ya vitu walivyojifunza kwenye kongamano:-

  • Jinsi ya kijana kujitambua
  • Jinsi ya kubadilisha unavyofikiria kama kijana wa leo na kufungua macho
  •   Mikakati iliyoandaliwa kuwaletea vijana maendeleo Mkoani Morogoro
  •  Mikakati iliyowekwa na kuonyesha fursa kwa vijana kama mikopo, kuboresha elimu zao, mbinu za kuwainua kiuchumi, kuwapatia ajira wasio na ajira na fursa nyingine nyingi kutegemea na kijana yuko wapi na anataka nini kwa wakati huo.
Picha za vijana waliohudhuria pamoja na waandishi wa habari
 
Picha ya Mkurugenzi wa Wezesha Trust Fund Bi Lusako Mwakiluma akitoa mada ya elimu ya utambuzi kwa vijana wajitambue na kujua thamani yao kabla ya kupata fursa
  
Mkurugenzi wa Victory Youth Support Organisation  Bw. Freddy Ng'atigwa  akielimisha vijana fursa zilizopo na jinsi ya kuzipata

JITAMBUE ILI UFANYE ULIYOKUSUDIA KUYAFANYA

 Neno jitambue ni kubwa na lenye kubeba maana nyingi kwa mtu yeyote anayekutana nalo, jitambue ni hali ya mtu kujifahamu yeye ni nani na anatakiwa afanye nini katika kila eneo la maisha yake.  
Kuna watu wanatembea lakini ukiwaangalia wamekata tamaa, wamezingirwa na mawazo lukuki yanayowafanya wasiwe na mawazo mapya katika fikra zao. Wamegubikwa na mambo mengi kiasi cha kujiona kwa nini wanaishi katika ulunwengu huu.
Watu wengi wamekuwa wepesi sana kukimbilia kwa rafiki zao ili kuomba msaada wa mawazo ya nini wafanye  kwenye maisha na hasa wakati wa shida.  Imani iliyojengeka kwa wengi katika jamii yetu ni kuwa, ushauri ni kitu muhimu sana kwa kila hatua.
Unaamka umenuna, unaoga umenuna, unavaa umenuna, unakwenda kazini umenuna. Jioni unarudi umenuna! Inasaidia nini? Kama una dukuduku na mke au mumeo, mwambie. Zungumza naye. Unanuna nini? Haitakusaidia kitu. Njia njema zaidi ya kumaliza matatizo ndani ya nyumba ni mazungumzo. Chukua hili kutoka kwangu.  
Hakuna kitu kibaya maishani kama kuonekana upo katika daraja la chini na mtu wa kudharaulika kwenye jamii unayoishi. Kisaikolojia kuna madhara makubwa.
Ni imani yangu kuwa kila mwanadamu timamu anapenda kuheshimiwa lakini wengi wetu tunashindwa kupata heshima tunayoitaka kwa sababu hatufahamu jinsi ya kuishi mbele ya wenzetu.
Watu wengi wamenifuata na kuniambia kuwa hawana furaha ya maisha. Niliwauliza kwa nini hawana furaha? Bila kusita kila mtu aliniorodheshea wingi wa shida zinazomkabili ambazo kwa namna moja au nyingine zimemfanya akose raha.
Lakini, je, kuwa na shida au mahitaji ya fedha ya matumizi, kuachwa na mume au kufiwa ni lazima iwe sababu ya mtu kukosa furaha? Mbona kuna wengine wanafurahia ujane kwa sababu tu wamebaki na mali za urithi?
Siku zote kikwazo cha furaha ya mwanadamu ni watu ingawa mazingira nayo huchangia kwa kiasi fulani lakini binadamu wenzake ndiyo adui namba moja wa raha ya mtu.
Tunaweza kujiuliza kwa nini watu ni tatizo? Jibu ni ni jepesi, mwanadamu hawezi kujihukumu kama hakuhukumiwa na wenzake. Katika hali ya kawaida, ukosefu wa furaha husababishwa na hukumu za watu ambazo huleta mawazo yanayoweza kumfanya mtu ajione duni.
Kitaalamu, ile hali ya kujiona mtu wa hali ya chini, uliyeshindwa kufanikiwa katika hili, uliyepitwa na wenzako kwa uwezo fulani, ndiyo huleta hali ya kukosa raha. Hii ina maana kuwa kukosa chakula chenye chumvi nyikani kusikokuwa na watu hakuwezi kukukosesha furaha kwa namna yoyote kama tu mawazo yako yanautetea udhaifu wako. 
Tabia kuu ya mwanadamu ni ulinganifu na wenzake, kile ambacho anaamini hajakipata ila mwenzake anacho ndicho huwa kikwazo cha furaha yake.  Hii ina maana kwamba tabia ya mtu kuwaza jinsi binadamu wenzake wanavyomfikiria ndiyo kisa ambacho humuondolea furaha.
Wakati wote tabia ya watu wasiokuwa na furaha huwa ni kufikiri namna ambavyo wenzake wanamfikiria. “Nimeshindwa kuendeleza duka langu, wenzagu si watanicheka?” Mawazo ya namna hii ya kuona wewe ni sehemu ya wale ndiyo mfereji wa kupoteza furaha yako.
Kwa kawaida, binadamu anapojifikiri mwenyewe bila kujilinganisha na wenzake hukubaliana na udhaifu wake na hilo haliwezi kuwa chanzo cha yeye kupoteza furaha yake.
Adamu na Hawa, wazazi wa kwanza wa binadamu kwa mujibu wa kitabu cha Biblia, hawakuuona udhaifu wao walipokuwa wakijifikiria wenyewe na nafsi zao mpaka nyoka alipowaletea mawazo ya kuazima kutoka kwa mtu mwingine ambayo yaliwageuza na kujiona wanyonge, wakatamani kuwa kama mtu.
Inaelezwa kwenye kitabu hicho kuwa, nyoka aliwauliza kama wanakubaliana na katazo la kutokula tunda la mti wa uzima ambapo wao walisema NDIYO, lakini waliporithishwa mawazo kuwa kuna mwingine anayewazidi ufahamu, waligeuka na kujiona wanyonge, wasiokuwa na utimilifu, wakosefu wa furaha na hivyo kuamua kula tunda si kwa sababu walipenda bali walitamani kufanana na mtu mwingine.
Ushauri wangu: Kama mtu anataka kuwa na furaha ya maisha anatakiwa kujifikiria zaidi mwenyewe na kuepukana na tabia za kukopa utu wa mwingine na kutamani kufanana naye. Mtu unaweza kuugua kwa muda, ukitulia utapona, unaweza kuwa maskini, lakini ukiacha kukata tamaa na kuongeza bidii utatajirika, hayo ndiyo maisha.
Kukosekana kwa jambo fulani unalolihitaji leo haina maana utu wako umepungua bali ni mapito ya maisha ambayo unatakiwa kukabiliana nayo wewe mwenyewe na mawazo yako na kuzishinda changamoto zote.
Kama ni mawazo ya kuazima basi lazima yawe yale ya kukusaidia mbinu za kushinda na si yatakayokufanya kujiona dhaifu mbele ya binadamu wenzako. Jipe moyo ushindi wa hayo yanayokukosesha furaha upo mikononi na akilini mwako.
Ni imani yangu kuwa kila mwanadamu timamu anapenda kuheshimiwa lakini wengi wetu tunashindwa kupata heshima tunayoitaka kwa sababu hatufahamu jinsi ya kuishi mbele ya wenzetu.
Kitaalamu, hakuna jambo ambalo hutokea maishani bila sababu maalumu hivyo hata kudharauliwa kwako au kwetu ndani ya jamii tunayoishi kunatokana na jinsi tunavyoenenda.
Watu waliopitia matatizo na shida duniani wameorodhesha  mambo mengi yaliyowafanya wawe kama walivyo, walipitia shida, walifeli, walishindwa na baadae wakajitambua na kuinuka na kuanza upya haujachelewa simama na anza tena utashangaa na kuwa ushuhuda kwa watu wengine. 
Watu wengi wanayaona mafanikio kwa watu weupe tu hapana, hata wewe unaweza kufanikiwa ukijitambua na ukiishi katika mtazamo wako na wala sio mtazamo wa mtu mwingine kwani kila mtu ana wazo lake na ana kipawa chake alichojaaliwa na Mungu na ndio maana unaweza kuiga mtu kuuza vitumbua kumbe sio karama yako kesho yake unaacha kwa kukosa uvumilivu wa kuungua na moto na harufu ya mafuta.
Simama katika nafasi yako na amua kuishi kwa jinsi unavyotaka wewe huku ukiwa na malengo yenye dhima ya kufikia ushindi wa hali ya juu sana.
Hakuna kinachotokea kwenye maisha yako bila kuwa na sababu, umezaliwa ili upambane na kufikia kilele cha hatima yako na siku zako za kuishi anajua yeye aliyekuleta hapa duniani.  Na mwisho wa siku zitatakiwa hesabu zake. Utaulizwa ulifanya nini kule ulikokwenda yaani hapa duniani.
 Ebu yaangalie haya hapa chini na kuyafanyia kazi kama unataka kujitambua na kuwa mahali pa kuheshimika katika jamii inayokuzunguka:-
MUONEKANO
Kwanza kabisa ni jinsi unavyoonekana. Muonekano ninaouzungumzia hapa ni usafi wa mavazi na mwili kwa ujumla. Hata siku moja hakuna mchafu anayeheshimika katika jamii anayoishi hata kama ana kipaji kikubwa kiasi gani.
Kwa hiyo uchafu wa mavazi na mwili huchangia mtu kudharauliwa katika jamii anayoishi. Linaweza kuwa jambo dogo sana lakini ni moja kati ya sababu kubwa inayochangia kuporomoka kwa thamani yako mbele ya wenzako.
Mazungumzo
Hapa naomba nieleweke kuwa unachokizungumza kinaweza kukujengea heshima au kukubomolea heshima. Kauli zisizo na busara zitakufanya udharaulike kwa kila mtu. Uropokaji usiokuwa na mantiki huchangia kuporomosha heshima yako hasa kama utakuwa muongeaji zaidi. Biblia inasema penye wingi wa maneno hapakosi uovu.
UTENDAKAZI WAKO
Ndugu zangu, siku zote heshima ya mtu ni kazi. Watu wengi hawapendi kufanya kazi kwa bidii huku wengine wakijiendekeza kwa tabia ya kuombaomba, jambo hilo halifai kwa vile huchangia kubomoa heshima yako mbele ya jamii. Fanya kazi usiishi bila kujishughulisha.
KUTOTIMIZA AHADI
Kama una tabia za kuahidi mambo halafu unashindwa kuyatekeleza, basi unajiweka katika nafasi mbaya ya kutunza heshima yako katika jamii unayoishi. Bora ukwepe kutoa ahadi kuliko kuahidi na kutotimiza.
SIFA ZISIZO NA MAANA
Nakumbuka msemo mmoja kutoka kwa mwandishi mwandamizi aliyekuwa mtaalamu wa falsafa za maisha, marehemu Adolf Balingilaki, ambao unasema kwamba:
“Ukitafuta heshima kwa gharama ya juu, basi utalipwa dharau kwa bei nafuu.”
Msemo huu unamaanisha nini? Siku zote ukiwa unafanya mambo yako kwa ajili ya kusifiwa au mazungumzo yako kuwa ya kujiinua, watu watakudharau.
KUTOKUWA MWAMINIFU
Suala la uaminifu ni pana, kuna uaminifu wa fedha, siri, dhamana na mambo kama hayo, hivyo ni vema kila unachoaminiwa lazima ukitunze kwani ukiwa mtu wa kuvunja uaminifu fahamu kuwa utashusha heshima yako.
Karibu tuelimishane na kusaidia pale unapojua niko tayari kujifunza toka kwako; naamini ili niweze kujua zaidi natakiwa kujifunza kupitia wenzangu.  
Karibuni sana tusonge mbele kwa ushindi.
Lusako Mwakiluma

CHARITY BEGINS AT HOME


Mkurugenzi wa Wezesha Trust Fund Bi Lusako Mwakiluma akiwa pamoja na wafanyakazi wenzake Ezma Mgaya(Afisa Maendeleo ya Jamii) na William Matajiri(Afisa Ugavi) wakitoa msaada katika kituo cha kulelea watoto yatima cha DAH-LUL Mkoani Morogoro kwa ajili ya kusherehekea pasaka, 2013
Wezesha Trust Fund ikikabidhi baadhi ya vyakula kwa Kituo cha watoto walemavu na wenye utindio wa ubongo Amani Centre – Morogoro –Kulia ni Mkurugenzi Bi Lusako Mwakiluma,  Mweka Hazina Bi Evetha Richard na Afisa Maendeleo jamii Bi Ezma Mgaya na kushoto ni Mkurugenzi wa Kituo cha Amani


WANAWAKE TUJITOE KUWASAIDIA WENGINE

Leo tarehe 8/3/2014 ni siku ya wanawake Duniani, wanawake wenzangu napenda kuwatakia siku njema na kuwatia nguvu kwa kuwapa hongera kila mwanamke kwa kuhadhimisha siku ya wanawake duniani kote: 
Napenda kuwaomba wanawake wenzangu tusiridhike na mafanikio madogo tuliyonayo: Ebu tujitoe kwa kazi za kujitolea katika jamii yetu ili kuweza kuwasaidia wanawake wenzetu wenye hali duni kuhakikisha wanapata nguvu za kuweza kusimama kwa kuwafundisha mbinu za kufanikiwa na kuinua hali zao hasa wasiokuwa nacho, wasiojiweza, walemavu na wajane na waishio katika hali ngumu.  Tusome kwa bidii kwa wale wasomi, na wale wajasiriamali wasimame katika sehemu zao kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya hali ya juu ili tukimbizane na soko la Kimataifa.
Wanawake wenye elimu tuzitumie elimu zetu kuwasaidia wasio kuwa na elimu kwa kuwafundisha jinsi ya kuwaelimisha wenzao, na pia kuwajengea misingi imara mabinti zetu walioko vyuoni na mashuleni  kwa kuanzia elimu ya awali kwa kuwashuhudia yale tuliyopitia sisi, ili kuwa chachu katika maisha yao ya leo na hata siku za usoni.  Changamoto na fursa tulizozipata kama wanawake wenye mwamko na mafanikio.
Utandawazi usiwe kigezo cha wao kuchukulia maisha kwa njia ya mkato tuwaelekeze kwamba wajitume sana na kufanya kazi kwa bidii popote walipo iwe mashuleni, majumbani, makazini na hata katika kazi za kujitolea. 
 Kwani unapotoa ndipo pale unapopokea wakitambua asiye fanya kazi na asile.
Tuwajengee uwezo  wa malezi; wazazi na walezi ili kuwanusuru  watoto na wasichana  kubakwa na  ndoa za umri mdogo zipigwe vita.
Kuwaelimisha wasichana na kuwapa fursa  wenyewe kutoa mawazo yao kuhusu udhalilishaji wa kijinsia mfano: Wale waliodhalilishwa na wale wanaotishiwa kudhalilishwa,  kutoa mbinu kwa wale ambao hawajakutana na hali hizo ili wajue mbinu za wadhalishaji na kujinusuru, na kutokuwa tayari kupokea zawadi ndogondogo zenye kuleta madhara.
Kuhakikisha wasichana na mabinti zetu  wanapata elimu ya kujitambua na kujithamini ili waweze kutimiza ndoto zao wasikwame njiani kwa majuto.
Kuhakikisha wimbi la ukeketaji linakwisha kabisa kwa kuwapa elimu wanaume kutosumbukia mabinti waliokeketwa na kuwapa mabinti hasara za ukeketaji.
Kuhakikisha tunawajengea uwezo makahaba na wanaofanya biashara haramu ya ngono kuwapatia elimu na mitaji ili waweze kujiajiri au kuachana kabisa na dhana ya ngono zembe kwa  kuuza mwili kwa faida ya pesa kidogo, yaani pesa ya kula leo tu. “Tuwafundishe kuvua samaki na sio kuwapa samaki wale na kesho wakaomba tena”.
Kuhakikisha wazazi na walezi wanapata stadi  za malezi yenye kuzingatia utandawazi bila kuharibu mila na desturi zetu tulizopitia sisi kwani ukimuelimisha mtoto wa kike umelielimisha Taifa kwa ujumla.  Watoto wasikurupuke kwa kuiga kwani kupitia kuiga ndio wanauandaa mwisho wao,  wanatakiwa wawe wabunifu wa vipaji vya wenyewe.
Changamoto wanazopitia wanawake wenzetu
Katika kuadhimisha siku hii tulikuwa pia tunaiomba serikali na wadau iwaangalie wanawake wenzetu wa kimasai, kisukuma na kikurya wanaopitia hali ngumu katika kufanya kazi kwa bidii kwa kuchunga kwa umbali mrefu, kutafuta kuni umbali mrefu, kupika, kufua, kuangalia watoto na  mwisho wa siku walaji ni wakinababa yaani wanaume kwa kudhalilishwa, kunyanyaswa na hata kukosa amani ndani ya nyumba zao wenyewe.
Wapewe msaada wa elimu endelevu ili na wao waweze kusimama katika jamii wakiwa wanawake wenye maamuzi ndani ya nyumba zao na pia wapatiwe elimu wenza wao yaani wanaume na kuelewa mwanamke ni mtu muhimu sana katika jamii yetu na kumpa nafasi ya kutoa maamuzi ndani ya nyumba zao na kusikilizwa na kupewa kipaumbele pale inapotakiwa kufanya hivyo.
Naamini kupitia siku hii wanawake wenzangu mtakuwa mmeamka kwenye blanketi zito la usingizi na kuanza kupiga hatua ili tuweze kuwa wasaidizi bora na sio bora wasaidizi.  Kwani katika kila mwanaume aliyefanikiwa yuko mwanamke nyuma yake.  Tuige mifano ya wamama kama Mama Obama, Dada yetu Oprah Winfrey, Mama Salma Kikwete na Mama Pinda tusimame daima kuhakikisha wanawake wanafanikiwa katika kila Nyanja Kiuchumi, kijamii, Kisiasa na Kielimu kwa kuelimishana na kufundishana kwa upendo na ukarimu tukijifunza kutoka kwa waliofanikiwa.
Mungu ibariki Tanzania, wabariki wanawake wote!!!!
Naomba tuamini kwa pamoja tunaweza.
Na: Bi Lusako Mwakiluma

JINSI YA KUMJALI MTEJA KATIKA BIASHARA YOYOTE


MTEJA ndiye mtu muhimu sana katika biashara yako. Hakuhitaji wewe ili kuishi, bali biashara yako inamuhitaji ili iendelee kudumu na wewe uweze kuishi. Kumbuka mteja wako asiporidhika, atakwenda sehemu nyingine atakaporidhishwa.
Kila wakati fahamu kwamba, mteja wako ni mtu muhimu sana ama awe amekuja yeye mwenyewe moja kwa moja kwenye biashara yetu au awe ametupigia simu au kutuandikia, tunapaswa kumjali na kumhudumia vizuri kama ipasavyo bila kuwa na visingizio!
Mteja hatuletei bughudha kwenye biashara yetu…yeye ndiye kusudi kuu la biashara yetu. Anatupatia upendeleo wa kipekee kwa kutupa sisi nafasi ya kumhudumia.
Mteja siyo mtu wa kubishana naye au kujaribu kushindana naye kwa maneno ili kumuonesha sisi ni wajuaji kiasi gani. Hakuna aliyewahi kushinda mabishano na mteja wake. Kwa namna yoyote mabishano makali yanaathiri  biashara yako. Tumia hekima na diplomasia kadiri iwezekanavyo.
Mteja ni mtu anayekuja kwetu kwa kuwa anahitaji huduma au bidhaa fulani hivyo ni kazi yetu kumtimizia mahitaji yake kwa njia ambayo ni ya faida kwetu na kwake pia.
Mteja siyo namba tu au takwimu, bali ni binadamu kama vile mimi na wewe. Ana hisia kama zile tulizonazo; hasira, furaha, njaa, kiu, uchovu, msongo wa mawazo, n.k.
Kutokana na haya machache niliyosema hapo juu, mteja ni mtu muhimu sana kwa biashara yetu, bila yeye biashara haiwezi kuwepo! Hivyo kama hujui namna ya kuwa mtaalam wa biashara yako, basi anza na sehemu hii muhimu ya biashara yako, halafu utapanua ufahamu wako kwa sehemu zingine.
Au kama umewaajiri wengine kwa ajili ya kushughulika moja kwa moja na wateja, basi hakikisha kuwa unawapatia maarifa haya kwa kupitia wataalam wa biashara, semina za ujasiriamali au wewe mwenyewe kuwafundisha, kuwahamasisha au hata kuwakumbusha kila wanaposahau.
Ni muhimu kufahamu kwamba watu wengi wanashindwa kila siku katika ulimwengu wa biashara kwa kuwa tu hawana maarifa katika vipengele mbalimbali vya biashara. Eneo jingine ambalo ni lazima uwe mtaalam bila kushindwa hata kidogo ni eneo la uuzaji. Ninaposema uuzaji nina maanisha uwezo wa kuwashiwishi wengine waweze kununua bidhaa yako, kukubali wazo lako au kujiunga na biashara yako.
Zamani nilipoanza kujifunza mbinu za kuwa tajiri kwenye ujasiriamali nilikutana na kanuni ifuatayo ambayo ni rahisi sana kuilewa:
Mauzo = Kipato.
Kwa lugha nyingine wewe kama mfanya biashara unapaswa kujiuliza mara kwa mara maswali kama yafuatayo:
“Nitawezaje kuongeza mauzo ya biashara yangu?”
“Nitawezaje kufanya hawa wateja nilionao waniletee wateja wengine zaidi?”
“Ni wapi ambako ninaweza kupata wateja wenye uwezo wakununua kwa wingi zaidi kutoka kwangu na kwa idadi kubwa kadiri iwezekanavyo?”
“Nitumie mbinu gani ili wateja wanapokuja kwenye eneo langu la biashara waweze kununua zaidi ya wanavyonununua sasa?”

Maswali kama haya mpendwa msikilizaji yana uwezo wa kubadilisha mapato kwenye biashara yako kuliko namna nyingine yoyote ninayoifahamu.  Hivyo tenga muda kila siku japo kwa nusu saa au saa moja, kuwa peke yako na jiulize maswali magumu kama haya, kisha andika  majibu kwenye kila kidaftari kidogo kila unapopata wazo jipya.
Kimsingi hii ndiyo siri kuu ya ushindi ya bilionea Richard Branson mwenye makampuni yenye nembo ya Virgin yanakadiriwa kuwa zaidi ya mia tatu ulimwenguni kote.
Mwingine ambaye siri hii ilimtoa ni ndugu Sam Walton ambaye ndiye mwasisi wa supamaketi za Wal-mart zilizozagaa ukimwenguni kote. Inasemekana kwamba wakati ndugu Walton anaanza biashara yake miaka mingi iliyopita kama mmiliki wa duka dogo tu lililouza vitu vya nyumbani alikuwa na tabia ya kwenda kujifunza.
Hivyo alijifunza walivyopanga bidhaa zao, walivyopunguza bei , walivyokuwa wakiongea na wateja n.k, Inasemekana kwamba Sam alikuwa ana tabia ya kuwahi kwenye supamaketi hizo asubuhi sana kabla hawajafungua na kupaki pick up yake nje na kusubiri wafungue.
Na mara tu walipofungua aliingia ndani na kidaftari chake kidogo na kuandika kila kitu alichojifunza ndani ya lile duka, aliporudi kwenye duka lake alijaribu kuiga mambo mengi kama alivyojifunza. Kwa lugha nyingine alikuwa ana copy na ku-paste!  Lakini yeye hakuishia hapo tu bali alikuwa ana-copy, halafu ana-improve na ku-paste. 

Leo hii japo Sam hayuko pamoja nasi amewaachia watoto wake utajiri mkubwa, wana maduka zaidi ya 8000 dunia nzima na wana mamilioni ya wafanyakazi ulimwenguni kote.

ZIELEWE CHANGAMOTO ZA MAISHA

 Kwa sababu tumeumbwa tofauti, wako walioumbwa kushughulika na mambo ya wenzao tu muda wote wanaangalia fulani kafanya nini na kafanikiwa au kashindwa kwa kiasi gani.  Mwisho wa siku ukiwaangalia watu hawa utajikuta unashindwa kufikia malengo yako na kukwama njiani katika safari yako ya maisha.  Ndugu yangu simama katika nafasi yako na usiwaangalie walioshindwa, walioshindwa wana maneno mengi sana.  Na ukiwafuata watakupotezea dira kabisa.  Amini kile unachokifanya na amini kwamba kitafanikiwa kwa asilimia mia moja pamoja na hali zilizopo usirudi nyuma Mungu ni mwema kwetu siku zote na yeye anaangalia mwisho wako sio mwanzo wako. 
 Kuna watu wameumizwa, kuna watu wameachwa, kuna watu wamekimbiwa na kuna watu wamefiwa na kukataliwa na kuonekana si kitu kwenye jamii zao zinazowazunguka.  Nakuomba ndugu yangu usifikirie kujiua au kususa kwa ajili ya maisha yako simama ukijipa moyo kwamba wewe sio wa kwanza unayepitia haya mama yangu nimpendaye sana Maya Angelou mwandishi wa vitabu na misemo yake mizuri alisema katika mahojiano yake na Oprah Winfrey “kwamba kila unachopitia amini sio wa kwanza kukipitia wapo waliopitia unayopitia tafuta njia mbadala na kisha endelea mbele” nakwambia muda sio wetu hata kwa kuuza maji ya mia mia utatoka tu.  Usikae chini na kukata tamaa utapoteza dira yako.
Hayo yaliyopita chukulia kama changamoto na hao waliokuacha na kukumbia wachukulie kama ngazi ya kupandia kuelekea kwenye mafanikio yako na yachukulie ya jana kama historia ya kuja kuwashuhudia watu waliokuwa na hali kama hizo kwa baadae.  Amina tu na songa mbele kwani adui ni ngazi ya kupandia na unaombwa kila siku kumpenda adui yako, jiulize je., huyu adui yangu akifa huyu nani atakuja kunipigia makofi wakati naenda kufanikiwa na kuwashuhudia wengine nilikotoka?.  Kuwa na roho ya unyenyekevu na ya msamaha kwa yeyote anayekwenda kinyume na wewe kwani hakuna barabara ndefu bila kona na hakuna yaliyo marefu bila kuwa na ncha.  Kumbuka kwa wale wakristo Danieli, Meshack na Abelnego waliwekwa kwenye tanuru na hawakuungua kwa sababu ya imani ya Mungu wao waliyemwamwini kwanini usiwe wewe ule moto ni changamoto kama hizi ninazokuhadithia hapa.  Naamini kuna watu wanaenda kupokea miujiza yao ya mafanikio kupitia changamoto hizi za maisha nasema maisha ni rahisi kama unayapatia na ni magumu kama unapoteza muda kuangalia tatizo badala la suluhisho la tatizo lako.  Jiulize Bill Gates, Obama, Hillary Clinton wao wamezaliwa na nani na wananguvu gani za kukushinda wewe ambaye una masaa hayo hayo na nguvu kama zao.  Inuka twende mbele tusipoteze muda wala saa.
Nakutakia usomaji mwema wa mada zangu na Mungu atakuinua kwa namna ya tofauti mpendwa. 
Karibu sana
Lusako Mwakiluma
 
Copyright © 2013 WEZESHA TRUST FUND
Powered by WordPress24x7