Leo
tarehe 8/3/2014 ni siku ya wanawake Duniani, wanawake wenzangu napenda kuwatakia
siku njema na kuwatia nguvu kwa kuwapa hongera kila mwanamke kwa kuhadhimisha
siku ya wanawake duniani kote:
Napenda
kuwaomba wanawake wenzangu tusiridhike na mafanikio madogo tuliyonayo: Ebu
tujitoe kwa kazi za kujitolea katika jamii yetu ili kuweza kuwasaidia wanawake
wenzetu wenye hali duni kuhakikisha wanapata nguvu za kuweza kusimama kwa
kuwafundisha mbinu za kufanikiwa na kuinua hali zao hasa wasiokuwa nacho,
wasiojiweza, walemavu na wajane na waishio katika hali ngumu. Tusome kwa bidii kwa wale wasomi, na wale
wajasiriamali wasimame katika sehemu zao kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na
viwango vya hali ya juu ili tukimbizane na soko la Kimataifa.
Wanawake
wenye elimu tuzitumie elimu zetu kuwasaidia wasio kuwa na elimu kwa
kuwafundisha jinsi ya kuwaelimisha wenzao, na pia kuwajengea misingi imara
mabinti zetu walioko vyuoni na mashuleni
kwa kuanzia elimu ya awali kwa kuwashuhudia yale tuliyopitia sisi, ili
kuwa chachu katika maisha yao ya leo na hata siku za usoni. Changamoto na fursa tulizozipata kama
wanawake wenye mwamko na mafanikio.
Utandawazi
usiwe kigezo cha wao kuchukulia maisha kwa njia ya mkato tuwaelekeze kwamba
wajitume sana na kufanya kazi kwa bidii popote walipo iwe mashuleni, majumbani,
makazini na hata katika kazi za kujitolea.
Kwani unapotoa ndipo pale unapopokea
wakitambua asiye fanya kazi na asile.
Tuwajengee
uwezo wa malezi; wazazi na walezi ili
kuwanusuru watoto na wasichana kubakwa na
ndoa za umri mdogo zipigwe vita.
Kuwaelimisha
wasichana na kuwapa fursa wenyewe kutoa
mawazo yao kuhusu udhalilishaji wa kijinsia mfano: Wale waliodhalilishwa na
wale wanaotishiwa kudhalilishwa, kutoa
mbinu kwa wale ambao hawajakutana na hali hizo ili wajue mbinu za wadhalishaji
na kujinusuru, na kutokuwa tayari kupokea zawadi ndogondogo zenye kuleta
madhara.
Kuhakikisha
wasichana na mabinti zetu wanapata elimu
ya kujitambua na kujithamini ili waweze kutimiza ndoto zao wasikwame njiani kwa
majuto.
Kuhakikisha
wimbi la ukeketaji linakwisha kabisa kwa kuwapa elimu wanaume kutosumbukia
mabinti waliokeketwa na kuwapa mabinti hasara za ukeketaji.
Kuhakikisha
tunawajengea uwezo makahaba na wanaofanya biashara haramu ya ngono kuwapatia
elimu na mitaji ili waweze kujiajiri au kuachana kabisa na dhana ya ngono zembe
kwa kuuza mwili kwa faida ya pesa
kidogo, yaani pesa ya kula leo tu. “Tuwafundishe kuvua samaki na sio kuwapa
samaki wale na kesho wakaomba tena”.
Kuhakikisha
wazazi na walezi wanapata stadi za
malezi yenye kuzingatia utandawazi bila kuharibu mila na desturi zetu
tulizopitia sisi kwani ukimuelimisha mtoto wa kike umelielimisha Taifa kwa
ujumla. Watoto wasikurupuke kwa kuiga
kwani kupitia kuiga ndio wanauandaa mwisho wao, wanatakiwa wawe wabunifu wa vipaji vya
wenyewe.
Changamoto
wanazopitia wanawake wenzetu
Katika
kuadhimisha siku hii tulikuwa pia tunaiomba serikali na wadau iwaangalie
wanawake wenzetu wa kimasai, kisukuma na kikurya wanaopitia hali ngumu katika
kufanya kazi kwa bidii kwa kuchunga kwa umbali mrefu, kutafuta kuni umbali
mrefu, kupika, kufua, kuangalia watoto na mwisho wa siku walaji ni wakinababa yaani
wanaume kwa kudhalilishwa, kunyanyaswa na hata kukosa amani ndani ya nyumba zao
wenyewe.
Wapewe
msaada wa elimu endelevu ili na wao waweze kusimama katika jamii wakiwa
wanawake wenye maamuzi ndani ya nyumba zao na pia wapatiwe elimu wenza wao
yaani wanaume na kuelewa mwanamke ni mtu muhimu sana katika jamii yetu na kumpa
nafasi ya kutoa maamuzi ndani ya nyumba zao na kusikilizwa na kupewa kipaumbele
pale inapotakiwa kufanya hivyo.
Naamini
kupitia siku hii wanawake wenzangu mtakuwa mmeamka kwenye blanketi zito la
usingizi na kuanza kupiga hatua ili tuweze kuwa wasaidizi bora na sio bora
wasaidizi. Kwani katika kila mwanaume
aliyefanikiwa yuko mwanamke nyuma yake.
Tuige mifano ya wamama kama Mama Obama, Dada yetu Oprah Winfrey, Mama
Salma Kikwete na Mama Pinda tusimame daima kuhakikisha wanawake wanafanikiwa
katika kila Nyanja Kiuchumi, kijamii, Kisiasa na Kielimu kwa kuelimishana na
kufundishana kwa upendo na ukarimu tukijifunza kutoka kwa waliofanikiwa.
Mungu
ibariki Tanzania, wabariki wanawake wote!!!!
Naomba
tuamini kwa pamoja tunaweza.
Na:
Bi Lusako Mwakiluma
Post a Comment